LHRC HQ: Justice Lugakingira House
+255 22 2773038 / +255 22 2773048

TAMKO KULAANI MAUAJI YA KIKATILI YALIYOTOKEA KATIKA SEHEMU MBALIMBALI NCHINI TANZANIA

  • TAMKO KULAANI MAUAJI YA KIKATILI YALIYOTOKEA KATIKA SEHEMU MBALIMBALI NCHINI TANZANIA
TAMKO KULAANI MAUAJI YA KIKATILI YALIYOTOKEA KATIKA SEHEMU MBALIMBALI NCHINI TANZANIA

TAMKO KULAANI MAUAJI YA KIKATILI YALIYOTOKEA KATIKA SEHEMU MBALIMBALI NCHINI TANZANIA

Taarifa kwa Vyombo vya Habari – 27 Januari 2022

Ndugu wanahabari, katika kipindi cha mwezi huu wa Januari, kumeripotiwa matukio mbalimbali ya mauaji ya kikatili, ambayo yameleta huzuni na kusababisha ukiukwaji wa haki za binadamu. Kituo cha Sheria ha Haki za Binadamu kimekusanya takribani matukio 20 ya mauaji hayo, yaliyoripotiwa katika mikoa ya Mtwara, Rukwa, Njombe, Katavi, Mwanza, Dodoma, Ruvuma, Dar es Salaam, and Mara.
Ndugu wanahabari, tukianza na mkoa wa Mtwara, mnamo tarehe 23 Januari mwaka huu kuliripotiwa tukio la askari polisi saba (7) ambao walikamatwa na Jeshi la Polisi na kufikishwa mahakamani kwa tuhuma za kumuua Bw. Mussa Hamisi Hamisi (25), mkazi wa Kijiji cha Ruponda wilaya ya Nachingwea mkoani Lindi.  Sababu za kuuwawa kwa Bw. Mussa ziliziripotiwa kuwa ni kitendo chake cha kudai fedha zake kiasi cha Shilingi Milioni 33.7 ambazo maaskari polisi hao walidaiwa kuzichukua baada ya kumpekua, na kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi mkoani Mtwara, ACP Marck Njera, mauaji hayo yalifanyika tarehe 5 Januari 2022. Mauaji haya ni mfano mzuri wa mauaji yanayofanywa na maafisa wa vyombo vya dola na kitendo hiki ni ukiukwaji wa haki ya kuishi. Kitendo cha kuchukua na kukataa kurejesha fedha za Bw. Mussa pia ni ukiukwaji wa haki ya kumiliki mali.
Ndugu wanahabari, katika tukio lingine lilitokea mkoani Mwanza, iliripotiwa kwamba wanawake watatu (3) waliuwawa na miili yao kutupwa katika eneo la Mecco Kusini wilayani Ilemela jijini Mwanza mnamo tarehe 20 mwezi huu. Ilidaiwa kwamba wanawake hao walibakwa kisha kuuwawa kikatili kwa kutatwa na mapanga na watu wasiojulikana. LHRC inalaani kitendo hiki cha ukatili dhidi ya wanawake na tunatoa rai kwa jeshi la polisi kufanya uchunguzi na kuhakikisha watu waliofanya vitendo hivi ya ukatili wanafikishwa mahakamani.
Ndugu wanahabari, mkoani Rukwa kuliripotiwa mauaji ya mama na watoto wake wawili wenye umri wa miaka 3 na 6 ambao waliuwawa katika mazingira ya kutatanisha na watu wasiojulikana, huku miili yao ikikutwa imekatwakatwa sehemu mbalimbali. Tukio hilo lilitotokea mnamo tarehe 24 mwezi huu katika Kijii cha Azimio-Katumba wilayani Sumbawanga.
Katika Mkoa wa Dodoma, tarehe 23 Januari 2022 kuliripotiwa tukio la watu watano (5) wa familia moja kuuwawa na watu wasiojulikana katika Kijiji cha Zanka wilayani Bahi. Tukio hilo lilithibitishwa na Jeshi la Polisi mkoani Dodoma na waliouwawa ni baba, mama, watoto wawili na mjukuu mmoja.
Pia, LHRC imerekodi tukio la mauaji Wilayani Songea mkoani Ruvuma, ambapo mhudumu wa nyumba ya kulala wageni ya Peace Lodge, Gema Haule (23), aliuwawa kikatili na mteja katika nyumba hiyo ya kulala wageni, ambapo mteja huyo alikuwa anadaiwa Shilingi 50,000. Kutokana na deni hilo, uongozi wa nyumba hiyo ya kulala wageni uliamua kushikilia simu ya mkononi ya mteja huyo aina ya Nokia na nguo zake hadi pale atakapolipa deni hilo. Hata hivyo, mteja huyo aligoma kulipa deni na kuendelea kuja mara kwa mara kudai vitu vyake. Mnamo tarehe 20 mwezi huu mteja huyo alifika tena kudai vitu hivyo na alipokatiliwa ndipo akaamua kutekeleza mauaji  hayo.
Jijini Dar es Salaam, mwanamke mmoja, Barke Pesa Rashid (30), aliripotiwa kuuwawa na mwanaume mmoja, Jonsiner Bounser (34), katika nyumba ya kulala wageni baada ya kukabwa shingo hadi kufa. Tukio hilo lilitokea tarehe 1 Januari mwezi huu eneo la Tabata Segerea. Kwa mujibu wa Jeshi la Polisi, Bw. Jonsiner alikula njama na mpenzi wa zamani wa mwanamke huyo, ambaye amefahamika kwa jina moja la White (33), ili amtongoze na kisha kumuua mwanamke huyo. Mara baada ya kufanya mauaji hayo, ambayo yanahusishwa na wivu wa kimapenzi, Bw Jonsiner alikiri kupokea malipo ya awali ya Shilingi milioni 1.2.
Mkoani Mara, tarehe 14 mwezi huu Bw. Daud Samwel (30), mkazi wa Kitongoji cha Burunga wilayani Serengeti, aliripotiwa kujinyonga kwa kutumia mkanda wa suruali yake baada ya kushindwa jaribio la kuwachinja watoto wake wanne (4) baada ya mke wake kundoka nyumbani na kumwacha mume wake na watoto kufuatia vipigo vya mara kwa mara. Baada ya kudhibitiwa na wananchi asitekeleze azma yake aliamua kujinyonga. 
Kituo cha Sheria ha Haki za Binadamu kinalaani vikali vitendo hivi vya ukiukwaji wa haki za binadamu. Kiufupi, vitendo hivi vya mauaji vimepelekea ukiukwaji wa haki kubwa mbili za binadamu, ambazo ni haki ya kuishi na haki ya kuwa huru na salama.  Matukio haya ya ukatili ni mwendelezo wa matukio mbalimbali ya mauaji na ukiukwaji wa haki za binadamu, husani haki ya kuishi na haki ya kuwa salama, ambayo yamekuwa yakiripotiwa katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwemo mauaji yanayotokana na wivu wa kimapenzi. 
Ripoti ya Haki za Binadamu ya mwaka 2020 inaonyesha kuendelea kushamiri kwa vitendo mbalimbali vya ukiukwaji wa haki ya kuishi, ikiwemo matukio 32 ya wanawake kuuwawa na wenza wao, ambapo kati ya hayo matukio 23 yalihusishwa na wivu wa kimapenzi. Pia kulikuwa na matukio manne ya mauaji yaliyofanywa na maafisa vya vyombo vya dola kutokana na matumizi ya nguvu kupita kiasi.
Ndugu wanahabari, ukiacha matukio ya watu kuuwawa kikatili, mwezi huu pia kumeripotiwa kupotea kwa watu kadhaa pasipokuwa na taarifa za mahali walipo. Mathalani, watu watano jijini Dar es Salaam waliripotiwa kutoweka mwishoni mwa mwezi Disemba na bado haijafahamika kilichowakumba na mahala walipo.
Tathmini iliyofanywa na LHRC imeonyesha kwamba sababu zinazochangia kutokea kwa matukio haya ya mauji na watu kujiua ni pamoja na wivu wa kimapenzi, imani za kishirikina, visasi, migogori ya mali, na afya ya akili. 
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kitaoa rai kwa Jeshi la Polisi kuongeza nguvu ya kuwatafuta na kuwafikisha mbele ya sheria wahalifu wote waliohusika na matukio haya ya mauaji. Wananchi pia watoe taarifa kuhusiana na vitendo vya kihalifu na ukiukwaji wa haki za binadamu ili hatua stahiki za kisheria ziweze kuchukuliwa. Hali kadhalika, viongozi wa dini wana nafasi kubwa ya kukemea vitendo hivi na kuwakumbusha watu na waumini wao kulinda uhai kama tunu na kuheshimu na kulinda haki za binadamu.
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu pia kinalipongeza Jeshi la Polisi kwa kuchukua hatua dhidi ya maaskari polisi saba waliotuhumiwa kumuua mfanyabiashara Mussa Hamisi Hamisi mkoani Mtwara na kuwafikisha mahakamani. Tunatoa rai kwa jeshi hili kuendelea kuchukua hatua stahiki dhidi ya maaskari wote wanaokiuka sheria na miongozo yao ya kazi.


Imetolewa leo Januari 27, 2021 na;
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC)

Anna Henga
Mkurugenzi Mtendaji

LEAVE A REPLY

Your email address will not be published.